“Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo imani pasipo matendo imekufa.”
— Yakobo 2:26
Leo tunakutana na ukweli wa moja kwa moja — Mungu hawezi kukupa kile ambacho huamini ataweza kukupa. Wengi wanajitangaza kuwa na imani: “Ninamuamini Mungu kwa kazi!” “Ninaamini kwa ndoa!” Lakini matendo yao ni kinyume kabisa!
Wanasema wanangoja mume kutoka kwa Mungu, lakini bado wapo kwenye uhusiano wa zinaa na “baby daddy” au ex. Wanapiga magoti kwenye madhabahu, lakini usiku wana booty call. Wanasema wanamuamini Mungu kwa kazi, lakini hawajawahi kufunga hata siku moja wala kushiriki program yoyote ya kiroho kuhusu eneo hilo.
- MATENDO YANASEMA ZAIDI YA MANENO
“Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.”
— Yakobo 2:18
Imani ya kweli huonekana kwenye hatua zako. Ukisema unamwamini Mungu kwa kazi, fanya programu ya kiroho kwa kazi hiyo. Si mara moja, si mara mbili — rudia, fuatilia, shikilia kwa bidii mpaka uelewe na kupokea kilicho chako.
Hatua zako zitasema kama kweli unaamini au unajifariji kwa maneno.
- MUNGU HATENDEI UBABAIFU — ANAITIKIA IMANI YA KWELI
Watu wanataka “deliverance” ya haraka, bila kujitoa, bila kumkubali mtumishi wa Mungu kwa dhati, bila kufuata maagizo ya kiroho. Lakini hata Yesu alikataliwa Nazareti, na hakuweza kufanya miujiza kwao — sio kwa sababu hakuwa na nguvu, bali kwa sababu walimkataa.
“Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni… yakunguteni mavumbi miguuni mwenu.”
— Mathayo 10:14
Ukitaka kufunguliwa, kubali mamlaka ya kiroho. Mpokee mtumishi wa Mungu kwa moyo wote, sio kwa nusu mioyo na mashaka. Hapo ndipo mlango wa neema unafunguka.
- USITARAJIE MAFANIKIO YA KIROHO KWA KULETA UBABAIFU WA MATENDO
Kama kweli unamwamini Mungu kwa mume au kazi:
- Funga uhusiano wa zinaa. Weka court order ya kiroho kwenye kiungo chako!
- Soma Neno la Mungu kila siku.
- Fanya programu za kiroho kwa bidii na ufuatiliaji.
- Toa sadaka kwa bidii.
- Mtafute Mungu kwa moyo wa kweli, sio kwa hisia.
Imani ya kweli haifichi aibu. Inavaa silaha za kiroho na kupigana mpaka matokeo yaonekane!
- LET GOD BE TRUE AND ALL MEN LIARS!
“Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo.”
— Warumi 3:4
Hata watu wakikwambia wewe huwezi, CV yako haijakidhi, hujafuzu — maneno yao ni uongo. Ikiwa unatembea kwa imani, utawashinda wote na Mungu mwenyewe atakuinua hadharani. Kuna watu walikukataa, walikudhihaki, walikula samaki mbele yako bila hata “karibu”. Lakini Mungu aliyekuwa kimya atajibu kwa kishindo!
- KAZI, MUME, AU NDOTO YOYOTE — JENGA KWANZA MSINGI WA IMANI
Kama hujui Neno la Mungu, huwezi kutangaza ahadi zake juu ya maisha yako. Kama hujafunga, hujasoma Zaburi, hujafanya programu yoyote ya kiroho — unaomba kutoka wapi?
“Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.”
— Yeremia 1:12
Mungu anatimiza NENO lake, si hisia zako. Hivyo kama ndani yako hakuna Neno — hakuna kitu cha kutimizwa. Jaza roho yako kwa Maandiko, shikilia ahadi zake, utashuhudia mikono yake ikifanya kazi maishani mwako.
- MUHIMU SANA — JIPIME!
Wewe wa Mei na wewe wa Januari — kuna tofauti gani? Kama hakuna hatua, basi hujafanya kazi ya kweli. Lakini kama umechimba Neno, umeomba kwa bidii, umejinyima na kujitakasa — basi toleo lako litakuwa na moto wa mbinguni juu yake.
SUNDAY CHALLENGE
Leo fanya tathmini:
- Je, imani yako ina matendo?
- Je, kweli unaamini Mungu kwa kazi au ndoa — au unajaribu kubet tu?
- Je, umempa Mungu nafasi ya kwanza, au bado wewe ni “boss” wa maisha yako?
Kama kweli umechoka na maisha ya kubabaika, anza leo kutembea katika imani yenye matendo. Utashuhudia miujiza!
“Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.”
— Yohana 8:32