USIWE NA UNAFIKI KATIKA ULIMWENGU WA ROHO – SIMAMA NA CONVICTION YAKO!
“Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; na wao waupendao watakula matunda yake.” – Mithali 18:21
Kila mmoja wetu anapitia siku nzuri na mbaya, lakini kinachotofautisha mshindi wa kiroho na aliyeanguka ni msimamo wake katikati ya changamoto. Dunia ya roho haihitaji waoga, wala wale wa kuingiza siasa za hisia. Ulimwengu wa roho haucheki, una rekodi ya maneno yako, una adhabu kwa kila tamko la upumbavu ulilolitoa ukiwa na hasira.
Wengi mnapenda kujihurumia mnapokuwa chini – mnalaumu, mnajitenga, mnatoa kauli nzito kama “Sitaki tena ndoa,” “Sitaki kusikia,” “Nimechoka na haya mambo,” kisha siku mbili baadaye mnarudi kwenye maombi mkisema, “Bwana nisaidie nipate ndoa!”
Unadhani Ulimwengu wa Roho Haukukusikia?
Ukijua unataka ndoa, sema hivyo bila kurudi nyuma. Kama uko serious, basi hata kama umeachwa kanisani saa saba mchana, saa nane unakuwa tayari unaomba, “Bwana, yule aliyekuja na akatoroka, asante – naomba mwingine mwenye nia ya kweli.” Hakuna kususa!
Wale wa zamani waliokataa kuinama kwa sanamu (Danieli 3:16-18), waliweka msimamo wao hata mbele ya tanuru la moto. Walijua wako upande wa Mungu hata kama moto utawateketeza. Je, wewe unayezunguka kwenye upumbavu wa kihisia, unaweza kusimama hivyo? Kama ungekuwa na tabia zao – Shadraki, Meshaki na Abednego – jina lako lingeandikwa kwenye historia ya kiroho pia.
UNAFIKI UNAOJIFICHA KWENYE HISIA UNATOA RUHUSA KWA SHETANI
Kauli zako za kukata tamaa, za kususa, za kurudi nyuma – ni ruhusa unayotoa kwa ibilisi. Umesema mwenyewe, “Sitaki tena,” umeandika, umetamka, umeapa. Na hizo ni hati ambazo adui anazitumia mahakamani mbinguni dhidi yako.
“Walimshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” – Ufunuo 12:11
Watu wa msimamo wanashinda kwa ushuhuda wao. Simama na ushuhuda wako hata kama unalia, hata kama moyo unapasuka vipande. Kama moyo wako umevunjwa mara 278, oga, lipaka mafuta, rudia sala yako – “Bwana, bado nataka ndoa.”
JE, UMECHOKA AU UMESHIKILIA?
Kama kweli umeamua kutafuta ndoa, shikilia hapo! Watu wa ukoo wako waliokubali hukumu ya mizimu waliona moto, wakasema, “Heri tuishi na mizimu kuliko huu moto!” Wewe unataka mwisho tofauti? Basi pita kwenye moto!
Simama! Kama una declare ndoa, sema hivyo usiku, mchana, saa nane, hata kama umeachwa, hata kama umedharauliwa! Wakati wengine wanacheka na kukubeza kwa sababu ya umri, rekodi yako ya maombi haibadiliki – “Bwana, bado nataka ndoa.”
HITIMISHO: UAMUZI WA MOYO NA MSIMAMO WA KIROHO
Shetani anaogopa mtu ambaye haongozwi na hisia, bali na uamuzi wa ndani wa kiroho. Wale waliomshinda hawakumshinda kwa kujipeleka mbele kwa machozi au lawama, bali kwa DAMU ya Yesu na USHUHUDA wa kinywa chao.
Ukikaza kusema kitu, kinaanza kuwa halisi. Ukiendelea kushuhudia, hata ukiwa unalia, ukweli wako unakuwa mwili.
Sema sasa:
“Bwana, mimi bado nataka ndoa. Sina aibu kusema. Nimepita mengi lakini bado nimesimama. Hakuna kurudi nyuma, hakuna kujichanganya. Mimi ni TEAM YESU hadi mwisho!”